Skip to content
Lifestyle

Tanzia Ya Mwalimu Gwiji Profesa Ken Waliaula Walibora

BY Juma · April 15, 2020 11:04 am

Marehemu Remmy Ongala alitunga wimbo maarufu wa Kifo Hakina Huruma. Kwa kweli, kifo hakina huruma hata chembe. Kifo ni kama zimwi, ni kama chatu ambaye kila uchao ni kuwang’wafua na kuwatafunilia mbali wanadamu ayani na ainati.

Kifo huvuna pasipostahili. Kifo huja bila barua ya mwaliko. Kifo hakimtambui tajiri wala maskini. Kifo hakiogopi. Huja bila kubisha hodi, tena kwa madaha na fujo na kumchukua mja bila ya tahadhari. Kifo ni dudu baya. Kifo huuma. Kifo huibadili siku njema ikawa balaa bin belua.

Leo hii, wapenzi wa lugha ya Kiswahi tumeraushwa na taarifa za kusikitisha za kifo cha mwalimu, muumbuji wa lugha ya Kiswahili, gwiji Profesa Ken Walibora. Bwana Walibora aliaga dunia siku ya Jumatano baada ya kupigwa dafrao na gari aina ya matatu.

Wanasema ajali haina kinga lakini ajali zingine huwa za kipuzi sana. Ajali ambayo imetupokonya Ken Waliaula Walibora ni ajali ya kipuzi sana. Lakini upuzi na upuzi huzaa mauti na sasa Ken hayuko.

Hivi sasa ni ukweli kwamba Ken Walibora hayupo nasi tena. Ameenda zake. Ameenda mbali kuungana na wazee waliomtangulia. Leo haikuwa siku njema kwake. Leo kidagaa chake kilimwozea na mbaya wake akampata na kumvunjilia mbali, mbali kabisa na uwezo wetu.

Anapoondoka Ken Walibora anatuacha sisi hoi. Majonzi sasa ni sehemu yetu. Nenda salama gwiji. Kawape salamu babu na bibi zetu waliotutangulia.

Kwale wale ambao hawana habari kumhusu Ken Walibora, itawabidi kutafuta baadhi ya kazi zake safi kama riwaya ya Siku Njema, ama kaitafute ile ya Mbaya Wetu. Na Ndoto ya Almasi Je? Kaisome ujionee. Tafuta pia mkusanyiko wa hadithi fupi wa Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine.

Kwa familia ya Ken, makiwa.

Juma is an enthusiastic journalist who believes that journalism has power to change the world either negatively or positively depending on how one uses it.(020) 528 0222 or Email: info@sokodirectory.com

Trending Stories
Related Articles
Explore Soko Directory
Soko Directory Archives